The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Maafisa Rasilimali Watu VETA waaswa kushughulikia changamoto za watumishi kwa weledi na wakati
Posted on: Thursday, 23 June 2022
Maafisa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wameaswa kushughulikia changamoto za watumishi kwa wakati na kwa weledi ili kupunguza malalamiko ndani ya Mamlaka.
Wito huo umetolewa, Jumatano, tarehe 22 Juni 2022 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, wakati akifungua kikao-kazi cha Maafisa hao kinachofanyika katika Chuo cha VETA, jijini Dodoma.
Amesema ushughulikiaji vyema wa changamoto za wafanyakazi unachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro na kuongeza tija na ufanisi kazini.
Amepongeza hatua ya uandaaji kikao-kazi hicho, akisema kuwa ni muhimu katika kujengeana uwezo, kupeana miongozo na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wa umma kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.
“Kumekuwa na mabadiliko ya sheria na miongozo mbalimbali inayohusu utumishi wa umma inayotolewa na Serikali. Ni muhimu kukutana na kupata fursa ya kuipitia, kuitafsiri na kupata uelewa wa pamoja na hatimaye kuitekeleza vyema,” amesema.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala VETA, Ndugu Felix Staki, ametaja baadhi ya mambo watakayojifunza na kujadiliana katika kikao hicho kitakachofanyika kwa siku nne kuwa ni pamoja na mabadiliko ya sheria na miongozo mbalimbali ya utumishi wa Umma, utaratibu wa kushughulikia masuala ya kinidhamu ya watumishi na namna ya kushughulikia malalamiko ili kupunguza malalamiko sehemu za kazi.
Amesema mada mbalimbali zitawasilishwa na wawezeshaji kutoka Tume ya Utumishi wa Umma.