The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Prof. Mkenda: Mageuzi ya Elimu nchini kuhakikisha Elimu Ujuzi inapatikana
Posted on: Saturday, 03 December 2022
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yanayokuja yanakwenda sambamba na kuandaa mazingira ya kuhakikisha elimu ujuzi inapatikana.
Mhe. Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja cha Menejimenti ya Wizara na ile ya VETA chenye lengo la kujadili kwa pamoja rasimu ya mkakati wa utekelezaji wa ujenzi wa VETA 63 za wilaya na moja ya mkoa.
Amesema moja ya eneo linaloangaliwa katika kutoa elimu ujuzi ni kupitia vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) hivyo ni vizuri kuwa na mikakati thabiti ya kuhakikisha VETA 63 za Wilaya na moja ya mkoa ujenzi unaanza.
"Nataka twende pamoja, katika kuweka historia hii; tunakwenda kufanya mageuzi makubwa ya elimu kwa kuhakikisha tunatoa elimu ujuzi, sasa kazi ya mapitio ya Sera na Mitaala inakwenda vizuri na tuko tayari kufanya wasilisho kwa ajili ya mjadala wa Kitaifa, sasa nataka huku kwenye ujenzi wa VETA 63 ambako elimu ujuzi inapatikana kuende kwa kasi na kwa wakati ,"amesema Prof. Mkenda
Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa VETA hizo hivyo kutaka mkakati wa kuhakikisha ujenzi unaanza mapema na kujengwa kwa usahihi kwa kuzingatia taratibu zote husika.
Akizungumzia maandalizi ya ujenzi wa VETA hizo Mkurugenzi wa Soko la Ajira, Mipango na Maendeleo wa VETA Mhandisi George Sambali, amesema mpaka sasa kati ya wilaya 63 zinazotarajiwa kujengewa vyuo vya VETA wilaya 59 tayari zimeshatenga maeneo yatakayo jengwa vyuo vya VETA.