Katika hali inayoweza kutafsiriwa kama kuendelea kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa ujuzi unaotolewa na vyuo vya VETA nchini kama suluhisho la ajira na maendeleo ya kiuchumi, wahitimu 73 wa shahada na 124 wa stashahada mbalimbali wameomba fursa ya kurasimisha ujuzi wao katika Mpango wa Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL) unaoendeshwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Katika awamu ya tatu ya Mpango huo ulioanza kutekelezwa kuanzia mwezi Juni 2020, jumla ya mafundi 34,818 waliopata ujuzi kwa njia ya uanagenzi bila kupitia mfumo rasmi wa mafunzo chuoni waliomba kurasimishiwa ujuzi wao ambapo wanagenzi 23,621 walikidhi vigezo.
Miongoni mwa wahitimu wa shahada na stashahada waliohojiwa juu ya msukumo wao wa kuomba kurasimishiwa ujuzi wao wametaja sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto za ajira, kupanua wigo wa fursa za ajira, kujiongezea kipato na wengine kwa mvuto walio nao kwa ufundi stadi husika.
Monica Baasa mkazi wa Dar es Salaam, mhitimu wa shahada ya Uhasibu aliyejifunza ushonaji kupitia mfumo usio rasmi anasema kuwa amepata hamasa ya kuomba kutambuliwa ujuzi wake ili kupata fursa mbalimbali hasa za mikopo, ambazo mara nyingi zinahitaji utambulisho rasmi wa shughuli ambayo mtu anaifanya.
Monica anaamini pia kuwa ujuzi wake ukirasimishwa na yeye kupata cheti atapata fursa ya kujiendeleza kimasomo kwenye fani ya ushonaji na hata kufikia kiwango cha kupata shahada kwenye eneo hilo kwani amekuwa na mvuto katika shughuli za ushonaji na ubunfiu wa mitindo ya nguo toka zamani.
“Imefikia hatua natamani hii shahada ya uhasibu igeuke na kuwa ya ushonaji lakini naamini kutambuliwa kwa ujuzi huu na kupata cheti cha VETA ni mwanzo mzuri wa kufikia malengo yangu,” anasema.
Naye Adam Omary, mkazi wa Morogoro, mhitimu wa shahada ya Ualimu ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Mbuyuni mkoani Morogoro aliyejifunza useremala kupitia mfumo usio rasmi amesema kuwa alianza kufanya shughuli za useremala mwaka 2002 baada ya kuhitimu kidato cha nne na alijifunza kwenye kiwanda kilichokuwa karibu na alipokuwa akiishi wakati huo.
Adam anabainisha kuwa lengo la kuomba kurasimishiwa ujuzi huo ni kutaka kuipa thamani shughuli yake ya useremala ambayo amekuwa akiifanya katika muda wake wa ziada lakini pia aweze kujiendeleza kwa kusoma ufundi stadi katika mfumo wa VETA ili baadaye aweze kuwa mwalimu wa fani ya Useremala.
“kazi ya useremala inanisaidia kwa asilimia kubwa kuendesha maisha yangu na ninaamini nikijiendeleza kwenye fani hii nitafikia malengo yangu,” anasema.
Shakira Juma, mkazi wa Dar es Salaam na mhitimu wa stashahada ya Ununuzi na Ugavi na mwenye ujuzi wa ufundi bomba, anasema kutambulika kwake kutamsaidia kupata kazi kwenye kampuni mbalimbali ambazo huhitaji utambulisho wa ujuzi husika kabla ya kutoa kazi kwa mwombaji.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, anasema ni jambo jema kuona kuwa watu wa makundi na viwango mbalimbali vya elimu wanazidi kutambua umuhimu wa ufundi stadi katika ujenzi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Anasema kuwa wahitimu wa kitaaluma katika ngazi mbalimbali wanaweza kunufaika kwa kupata mafunzo ya ufundi stadi, hata yakiwa ya muda mfupi, kama nyenzo ya kuwawezesha kuanzisha shughuli zao au kusimamia kwa ufasaha utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi.
“Mtu mwenye stashahada au shahada anakuwa amepanua ufahamu na uwezo wake wa kupambanua mambo. Kwa hiyo, akijifunza ufundi stadi, anaweza hata kuanzisha kiwanda kidogo au mradi mwingine na kufanikiwa vizuri. Ataweza kujiajiri na kuzalisha ajira,” anasema.
Mpango wa Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (RPL) unawahusu watu wenye ujuzi uliopatikana bila kupitia chuoni (Wanagenzi) ambapo hufanyiwa tathmini ya ujuzi wao, kuandaliwa mafunzo ya kuziba mapungufu waliyonayo na kisha kutambuliwa na kutunukiwa vyeti.
Mpango huu una lengo la kuwasaidia wanagenzi kupata kazi zenye staha na kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika soko la ajira; kuinua tija mahali pao pa kazi na kusaidia waajiri kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu. Ni zoezi ambalo linakwenda sambamba na lengo la kuandaa nguvu kazi kwa ajili ya uchumi wa viwanda.
Katika kipindi kati ya mwaka 2010 na 2019, jumla ya wanagenzi 10,023 walirasimishiwa ujuzi wao na kutunukiwa vyeti katika Mpango uliofadhiliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kati ya mwaka 2010 hadi 2016 na baadaye Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu mwaka 2017 hadi sasa.
Zoezi la Urasimishaji Ujuzi lililotangazwa na VETA mwezi Juni mwaka huu, litatekelezwa kwa awamu, ambapo litaanza na wanagenzi 6,243 kati ya 23,621 waliochaguliwa na wengine 17,378 waliobaki kurasimishwa katika awamu zinazofuatia.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office