The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Maafisa Ununuzi na Ugavi VETA wakumbushwa weledi na uadilifu katika kazi
Posted on: Monday, 13 March 2023
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewakumbusha Maafisa Ununuzi na Ugavi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli za Mamlaka hiyo.
CPA Kasore ametoa wito huo tarehe 11 Machi, 2023 wakati wa kikao kazi kati ya Menejimenti ya VETA Makao Makuu na Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wa Kanda na vyuo vya VETA nchini kilicholenga kujadili utekelezaji wa shughuli za kada hiyo na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi.
CPA Kasore amesema wataalamu wa ununuzi na ugavi wana mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya VETA na kwamba ni muhimu wakatekeleza kazi zao kwa kuzingatia misingi na taratibu za taaluma yao na taratibu za utumishi wa umma.
“Napenda kuwakumbusha umuhimu mlionao katika kufanikisha shughuli za Mamlaka ambazo ni za kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa watanzania…Nawasihi sana mtekeleze majukumu yenu kwa ufanisi ili kutokwamisha shughuli za Mamlaka na hatimaye kufanikisha malengo tuliyojiwekea,” amesema
Aidha, CPA Kasore amewaasa Maafisa hao kutoa ushauri wa kitaalamu mara kwa mara ili kuwasaidia viongozi kwenye maeneo yao kufanya maamuzi sahihi na kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo.
Awali, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa VETA, Bi. Witness Mgimba, amesema utendaji kazi bora wa maafisa ununuzi na ugavi utasaidia kuongeza tija kwenye Mamlaka hiyo na kuwataka Maafisa hao kuzingatia ufanisi, uadilifu na weledi.
Bi. Mgimba amewasihi maafisa ununuzi kujiongeza kwenye kazi zao kwa kujifunza masuala mbalimbali kuendana na mabadiliko yanayotokea kwenye taaluma hiyo na kuwataka kuwa na utayari wa kupokea mawazo na ushauri wenye lengo la kuleta ufanisi katika shughuli mbalimbali.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Maafisa Ununuzi na Ugavi 45 kutoka ofisi za kanda na vyuo vya VETA pamoja na watendaji waandamizi wa Mamlaka hiyo.