The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
UJENZI WA JENGO LA OFISI ZA VETA MAKAO MAKUU JIJINI DODOMA WAANZA
Posted on: Sunday, 25 June 2023
UJENZI WA JENGO LA OFISI ZA VETA MAKAO MAKUU JIJINI DODOMA WAANZA
Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) umeanza rasmi leo, baada ya Mkandarasi kukabidhiwa eneo la ujenzi lililopo Medeli jijini Dodoma.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 24 Juni, 2023 baina ya kampuni ya ABECC Ltd ambaye ni Mshauri Elekezi aliyewakilishwa na Mkadiriaji Majenzi, Novatus Mikapagaro na Kampuni ya ujenzi MOHAMMEDI Builders Ltd aliyewakilishwa na Mhandisi Ujenzi, Josephat Loya, na kushuhudiwa na Menejimenti ya VETA ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, CPA. Anthony Kasore.
Ujenzi wa jengo hilo litakalokuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya ofisi, maegesho ya magari, kumbi za mikutano na maktaba unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 12.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, amesema VETA itatoa ushirikiano utakaohitajika katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo na kuwasisitiza watekelezaji wa mradi kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa ubora, ufanisi na kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.
Wafanyakazi wa VETA Makao Makuu walihamia jijini Dodoma mwaka 2021 ambapo wamekuwa wakitumia majengo ya ofisi za VETA Kanda ya kati kutekeleza shughuli za Mamlaka hiyo.