The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amesema Serikali imejidhatiti katika kuhakikisha Watanzania wanapata ujuzi utakaowawezesha kufanya shughuli za kiuchumi kwa weledi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Buhigwe katika eneo la Ruheka Wilayani Buhigwe, tarehe 17 Septemba, 2021, Mhe. Majaliwa amesema ili kufanikisha mpango huo, Serikali imefanya uamuzi wa kuhakikisha inajenga chuo cha ufundi stadi kila Wilaya nchini ili kuwezesha wananchi kupata mafunzo hayo katika maeneo waliyopo.
"Mkakati wetu ni kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na ujuzi unaomwezesha kutenda kazi kwenye eneo analoweza kusimamia" Amesema.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu na hasa mafunzo ya ufundi stadi na kuahidi kuwa Wizara yake itasimamia ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyuo vya VETA vya Wilaya ili kuhakikisha inakamilika kwa ubora uliokusudiwa.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Chuo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu, amesema ujenzi wa chuo hicho ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuwasogezea wananchi wake huduma muhimu za mafunzo ya ufundi stadi kwa kuhakikisha kunakuwa na chuo cha Ufundi Stadi katika kila Wilaya nchini.
Dkt. Bujulu amesema chuo hicho ni kati ya vyuo 29 vya Wilaya vinavyojengwa nchini kwa utaratibu wa kutumia nguvu kazi ya ndani (Force Account) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa ESPJ (Education and Skills for Productive Jobs), na kwamba mradi huo unatekelezwa na VETA kupitia Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kigoma (VETA Kigoma).
Amesema kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 70 ambao hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 2.48. Chuo hicho kikikamilika kitatoa mafunzo katika fani sita ambazo ni Ushonaji na Ubunifu wa Mavazi, Uhazili na Matumizi ya Kompyuta, Uashi, Umeme wa Majumbani, Ufundi Magari pamoja na Uchomeleaji na Uungaji Vyuma.
Kwa mujibu wa Dkt Bujulu, chuo cha VETA cha Wilaya ya Buhigwe kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa wanafunzi 240 pamoja na mafunzo ya muda mfupi kwa wanafunzi zaidi ya 960 kwa mwaka.
Dkt Bujulu ametaja baadhi ya changamoto za utekelezaji wa mradi huo kuwa ni pamoja na kutopatikana kwa vifaa vya ujenzi Wilayani Buhigwe, hivyo kulazimika kuvinunua Kigoma Mjini au Kasulu, hali iliyosababisha ongezeko la gharama za ujenzi na kupungua kwa kasi ya utekelezaji wa mradi.