The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WARATIBU WA MAFUNZO VETA WANOLEWA USIMAMIZI, UENDESHAJI WA MAFUNZO YA UFUNDI STADI KWA UFANISI
Posted on: Wednesday, 07 June 2023
WARATIBU WA MAFUNZO VETA WANOLEWA USIMAMIZI, UENDESHAJI WA MAFUNZO YA UFUNDI STADI KWA UFANISI
Waratibu na Wasajili wa vyuo vya VETA wamekutana jijini Dodoma kwa lengo la kujengewa uwezo katika kuboresha usimamizi na uendeshaji wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Kikao kazi hicho kinachofanyika kwa siku mbili katika Chuo cha VETA Dodoma, kimefunguliwa rasmi leo tarehe 7 Juni, 2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Ndg. Abdallah Ngodu akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA.
Ndg. Ngodu amewataka waratibu na wasajili hao kufuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizoandaliwa na kutoa maoni yao na hatimaye kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Mwakilishi wa Waratibu wa Mafunzo kutoka VETA Kanda ya Magharibi, Ndg. Charles Mpambwe, ameshukuru Uongozi wa VETA kwa kuandaa kikao kazi hicho ambacho amesema kitatumika kama sehemu muhimu ya kupeana mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za utoaji mafunzo kwenye vyuo vya VETA na kubadilishana uzoefu ili hatimaye kuleta ufanisi katika mafunzo.
Miongoni mwa mada zinazowasilishwa kwenye kikao kazi hicho ni upangiliaji wa karakana na mazingira (Kaizen model), taarifa ya Mitaala iliyohuishwa, taarifa ya ufuatiliaji na tathmini ya mafunzo, miongozo ya ufundishaji wa elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na taarifa ya utoaji mafunzo ya uanagenzi.